Manusura wa Mporomoko Wa Ardhi Eneo la Mlima Elgon, Wapanda Miti 30,000 Kupitia Akiba ya Kikundi cha Kijiji, Ili Kupambana na Tabia Nchi

Na Javier Silas Omagor

Miaka mitano iliyopita wakati Musa Mandu alimufahamisha mke na jamii yake kwamba atawachana na kazi yake ya serikali ya mtaa ili apambane na tabia nchi wilayani Manafwa, walisikitika sana.

“Hawakuelewa maana yake ni nini. Hawakudhania kwamba hii ingeniwezesha kujimudu na kumudu jamii yangu kifedha,” Mandu alisema. “Haikuwa na bado sio kitu ambacho watu wanadhania kinaweza kuleta riziki. Hakuna yeyote, haswa miongoni mwetu sisi watu wakawaida, anayeelewa manufaa itokanayo na uhifadhi wa mazingira.”

Hata hivyo, aliyekuwa mekanika wakati mmoja hakuyatilia maanani wasiwasi wa mke na jamaa zake, ila alifungua shirika la akiba na mkopo kijijini lijulikanalo kama Bubulo Environmental Conservation Management Association (BECOMAP). Mradi huu ulizinduliwa kwa lengo la kuhifadhi mazingira ndani ya wilaya ya Manafwa na maeneo jirani. Wanachama wa kikundi humudu maswala yao wenyewe, huku wakiweka akiba ambayo huitumia kutoa mkopo kwa kila mmoja wao kwa kiwango cha riba cha chini.

“Katika eneo hili letu (kijiji cha Namutembi), nilitaka kuhakikisha ya kwamba wanavijiji walielewa umuhimu wa kuyapa kipaumbele maswala ya mazingira, katika yote tunayojihusisha nayo kama wenyeji, hata kufikia utungaji sera, na kwamba hatujihusishi tu na ulindaji mazingira, bali pia tunahakikisha kwamba tunaboresha maisha yetu tukiwa na hali dhabiti ya kifedha,” Mandu alisema.

Suluhu za kijamii dhidi ya maporomoko

Uanzilishi wake ukifanyika mwaka wa 2013, mradi huu ulilenga kuhamasisha wakaazi kuweka akiba kwa matumizi ya upanzi miti, kuregesha hali kawaida ya kingo za mito na uhamasishaji jamii kwa madhumuni ya kudhibiti mafuriko, momonyoko wa udongo, ulowaji maji, na maporomoko ya ardhi. Mandu na wengi wa wanachama wa kikundi ni manusura wa maporomoko ardhi na mafuriko ya hivi karibuni, ambayo yameadhiri eneo la Mlima Elgon kwa miaka mingi imepita, haswa katika wilaya za Bududa, Manafwa, Sironkho na Bulambuli.

Historia ya maporomoko katika eneo hili ni ndefu. Milioni kumi na moja meta mcheraba ya mafusi yalibingirika kutoka mteremko wa Mlima Elgon katika miaka ya 1950 na mwazo wa miaka ya 60, yakiishia mitoni na vijitoni. Thelathini ya maporomoko haya yaliziba mito, huku yakiharibu madaraja na barabara wakati maji haya yalivunja kingo za mito.

Hata hivyo, maporomoko haya yameongezeka na adhari zake kukidhiri katika miaka ya hivi karibuni. Kati ya mwaka wa 1997 na 2004, mvua kubwa ilisababisha vifo vya watu 48 huku watu kumi elfu wakilazimika kuhama na kubaki bila makao, katika eneo kubwa la Manafwa. Katika mwezi wa Machi, mwaka wa 2010, maporomoko katika kijiji cha Nametsi, wilayani Bududa, ambayo imebakia kuwa kisa kibaya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Uganda, yalipelekea watu 100 kuaminika kufa, wengine 300 kutoweka na maboma 85 kuharibiwa.

Katika mwaka wa 2018, maporomoko zaidi yalisababisha vifo vya watu 60, huku wengine 400 wakitoweka na mali ya dhamani ya mabilioni ya fedha yakisukumwa na mafusi. Shirika la Red Cross Society nchini Uganda ilikisia watu 12,000 kuadhirika katika mwaka wa 2018 katika kaunti ndogo za Bukalasi na Buwali huko Bududa.

Mvua isiyo ya kawaida katika miaka ya hivi karibuni ndio sababu ya maporomoko mengi, kwa mujibu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini Uganda. Nyingi ya maporomoko haya hufanyika katika miteremko mikubwa iliyobonyea ambamo maji hukusanyika. Miteremko inayotazama upande wa kaskazini mashariki ndio iliyo na hatari kubwa ya kuporomoka, ambayo inasadifikiana na upande ule mvua hunyesha mara nyingi.

Mbinu duni za ukulima, pamoja na uharibifu wa kingo za mito na vijito, vimezidisha pakubwa mikosi hii.

Katika miaka ya 1960, 1970 na 1980, maji ya mito wilayani Manafwa kama vile ile ya Paasa, Nametsi na ya mto Manafwa yalikuwa masafi na salama kutumika na jamii kwa maishilio yao. Milima, mabonde na miteremko daima ilitanda na mimea ya kijani kibichi kama vile nyasi na miti. Ila kwa sasa, kutowajibika kwa watu kwenye shughuli zao, zimewacha miteremko hii kuwa wazi, huku kingo za mito na vijito kuharibiwa, hivyo  kupelekea kulegea kwa udongo, jambo ambalo huchangia visa vya miporomoko.

Wasiwasi wa kuongezeka kwa hatari, ilimfanya Mandu na wakaazi kumi wa Namutembi, kata ya Bubwaya jijini Manafwa kuzindua BECOMAP mwaka wa 2013, ili kulinda mazingira na maisha ya watu katika eneo hili.

Kila mwanachama alitoa mchango wake wa UGX 20,000 ama 50,000 (USD 5- USD 13). Kila mmoja wa wanachama kumi anzilishi  walihitajika kutoa ekari moja ya ardhi kwa madhumuni ya upanzi wa miti 100.

Kwa muda wa miaka sita iliyopita, kundi hili limepanuka hatua baada ya hatua na kufikia wanachama 72 waliosajiliwa, huku asilimia 20 miongoni mwao wakiwa vijana na asilimia 30 wakiwa wanawake. Miti 30,000 tayari imeshapandwa na kundi hili. Mradi huu umekalia eneo la ekari 50 ya ardhi, ambayo inamilikiwa na jamii chini ya mkataba wa maelewano.

Kwa kawaida, kundi hili hupanda miti asili iliyokuwa inapandwa nyakati jamii zilizingatia utamaduni wa Kiafrika. Hii ni pamoja na aina ya miti kama vile Mvule, kando na msonobari na mkalitusi, kwa kuwa mizizi ya miti asili inasitiri udongo na maji na hupandwa kati ya mazao mengine shambani.

Upanzi wa misitu imekuwa ni chanzo cha pato kubwa kwa jamii. Kando na upanzi miti, kundi hili linajishughulisha na kilimo mseto ndani ya misitu yao katika kukuza nafaka, mboga kama vile kabeji, nyanya na parachichi pamoja na matunda kama vile pasheni na maembe kwa madhumuni ya biashara na ulaji mabomani. Kundi hili pia huuza miti kwa sababu ya mbao na lina pia mizinga ya nyuki ndani ya misitu hii, inayozalisha asali ambayo wao huuza, Mandu asema.

Kwa kadiri, wao hujipatia pato la UGX 1M – 1.5M (USD 270-405) kila wiki, huku asali ikiwa ndio bidhaa inayouzwa kwa wingi katika na mradi wa upanzi miti katikati ya mazao.

John Wabuna, kijana wa umri wa miaka 20-na, alisema kuwa vijana kama yeye katika jamii sasa waweza kumudu karo yao ya shule kutokana na uuzaji wa asali, matunda, mboga na mbao.

Wapo vijana 15 waliojisajili rasmi kuwa wanachama wa BECOMAP, huku 50 wengine wakijishughulisha na kampeni.

Kikundi kinasema kwamba, maafa asilia yalikuwa ni changamoto kubwa katika eneo hili, lakini yamepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya misitu. Hii ni tofauti na hali ilivyo ndani ya wilaya jirani za Bududa, Namisindwa na Butaleja ambako mvua ya gharika huchochea majanga mabaya.

Mandu alihimiza jamii zote nchini Uganda kukumbatia bila kisingizio chochote mtazamo huu walio nao, ili wapate kupigana kikamilifu na tabia nchi.

Katika siku zinazokuja, BECOMAP inatazamia kukibadisha kikundi kutoka kuwa kile cha akiba tu na kuwa shirika la kijamii kinachopigana na mabadiliko ya tabia nchi katika eneo la Mlima Elgon miongoni mwa maeneo mengine. Hii ni kwa mujibu wa Michael Mirisio, msimamizi wa ya utendaji na mikakati.

Kulingana na ripoti ya idara ya maendeleo ya kimataifa ya ReliefWeb, mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na binadamu, huenda yakaongeza kiwango cha joto nchini Uganda kufikia hadi 1.50C katika miaka ishirini ijayo kando na kiwango hiki kupanda hadi 4.3oC kufikia miaka ya 2080. Ongezeko la viwango hivi havijawahi kuonekana kamwe.

Mabadiliko ya vielelezo vya mvua na kiwango cha mvua kila mwaka pia vinatarajiwa, ambazo zitaadhiri kilimo, uti wa mgongo wa uchumi wa Uganda.

Ripoti hii inadhirisha wazi kwamba mabadiliko ya tabia nchi inahatarisha Uganda kwa kiasi kikubwa– nchi ambayo uchumi na maslahi ya wananchi wake inawiana sana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na binadamu katika karne ijayo huenda yakasitisha ama kuregesha nyuma mwelekeo wa nchi kimaendeleo.

“Wanasiasa na wanabiashara mashuhuri lazima washirikiane katika mapambano haya; haiwezekani kudhalalisha ulimwengu na watu wake kisha wafanywe watumwa wa kuchimba madini yake, kulima udongo wake na kutarajia kuunda uchumi endelevu duniani. Ulimwengu wako tajiri utaangamia, nyauka, fifia na kuporomoka,” alitahadharisha Rhoda Nyariibi, afisa wa kimazingira, manispaa ya Mbale.

Mabadiliko ya tabia nchi haswa katika eneo la Mlima Elgon, huenda ikamaanisha kwamba, maisha na mali ya watu yatapotea, huku hali ya usalama wa chakula ikidorora zaidi, mabadiliko katika kuenea kwa magonjwa kama vile malaria, momonyoko wa udongo na kuzorota kwa ardhi, uharibifu wa miundo misingi na makao utokanao na mafuriko, mabadiliko ya uzalishaji wa kilimo na raslimali.

Je, miti inapambana vipi na mabadiliko ya tabia nchi?

“Mabadiliko ya tabia nchi na kupanda kwa halijoto duniani inahatarisha ulimwengu mzima hivi leo, kwa vile hatuwajibiki jinsi ambavyo tunaingiliana na mazingira. Hata hivyo, sisi kama wanadamu, tunaweza chukua hatua zinazostahili kwa mafunzo ya maisha,” Mandu alisema.

“Nafikiria kila mtu sasa ameona jinsi misimu inavyobadilika, huku kiwango cha joto kikiongezeka na kile cha maji kikipungua kwa kiasi kikubwa. Hii inamaanisha kwamba, tunahitaji kuchukuwa hatua sasa. Haitulazimu kutegemea uingiliaji kati wa serikali,” alisema.

Nyingi ya miti ya BECOMAP inapandwa kando kando ya mabonde, miteremko, vijito na kingo za mito ili kudhibiti miporomoko ya ardhi, mafuriko na uloaji maji, ambayo ni matukio ya mara kwa mara kwenye miteremko ya Mlima Elgon. Bali na kupunguza majanga, miti huondoa hewani dioksidi kabonia na aina nyingine ya gesijoto, ambayo hupunguza adhara za mabadiliko ya tabia nchi.

Fredrick Jordan Oluka, mtaalam wa maswala ya mabadiliko ya tabia nchi ambaye pia ni mwanajiolojia, alisifu mikakati ya BECOMAP, akieleza kwamba umuhimu wa miti ni mkubwa mno katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Kiwango cha joto katika jamii ambazo zipo chini ya kivuli huwa 6-100F chini ikilinganishwa na za jamii ambazo hazina miti, hivyo kupunguza ile hali ya kisiwa-cha-joto huku ikipunguza mahitaji ya nishati,” Oluka alisema. “Upanzi wa miti ni zoezi rahisi ambalo yeyote yule anaweza kutekeleza hivyo kupunguza kiwango cha dioksidi kaboni, mojawapo ya gesijoto zizochangia pakubwa hali ya mabadiliko ya tabia nchi.”

Oluka, anashukuru BECOMAP haswa kwa kutilia maanani upanzi wa miti kando kando mwa vikingo vya mito, miteremko na mabonde, kwa kuwa miti mingi inayotumika ni imara ambayo hushikilia udongo na mawe pamoja, hivyo kuzuia kutokea kwa majanga kama vile miporomoko ya ardhi.

Mtaalam huyu wa maswala ya mabadiliko ya tabia nchi alisema kwamba punde miche hii itakapokomaa kwa muda wa miaka 10 ijayo, itasaidia kudhibiti udongo, huku ikikatiza upepo na ikichangia faida zaidi zinazoendeleza mazingira.

“Hivyo basi, hii inamaanisha kwamba eneo la Mlima Elgon hivi karibuni litashuhudia kupungua kwa visa vya miporomoko ya ardhi na momonyoko wa udongo kwa ujumla,” Oluka alisema.

Dkt. Arthur Bainomugisha, mwenyekiti wa muungano wa Coalition Development and Environment (ACODE), alikisifu kikundi kwa kutetea uhifadhi wa mazingira katika miteremko ya Mlima Elgon.

Bainomugisha alisema kwamba angependa kuona kila jamii nchini Uganda ikiiga mfano wa BECOMAP ili kulinda siku za usoni za nchi hii katika nyakati hizi zisizotabirika.

“Katika nchi zilizoendelea, upanzi wa miti hutekelezwa hata mijini na majijini, kitu ambacho hakifanyiki katika mataifa yanayoendelea. Hii ni inatokana na sababu kwamba, miji iliyo na vivuli hupunguza joto katika maeneo ya uegeshaji magari, hivyo kupunguza uzalishaji gesi kutoka kwa matangi ya mafuta, vituo vya mafuta na injini za magari, hivyo kupeleka kupungua kwa hali ya kisiwa-joto miongoni mwa jamii,” Bainomugisha alisema.

Bainomugisha alihimiza kila jamii nchini Uganda kukumbatia muelekeo wa BECOMAP. “Huenda pia ikasaidia haiba ya Uganda kimataifa kwa kuwa, wakati wa kongamano la Umoja wa Mataifa wa 2016 wa mabadiliko ya tabia nchi mjini Marrakech, Morocco, ilibainika kwamba Uganda ni mojawapo ya nchi ambazo hazijajizatiti kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema.

Sam Mauso Sirali, mmoja wa waanzilishi wa BECOMAP ambaye pia ni mwanauchumi aliyestaafu, alisema “haijalishi unapoishi, waweza panda miti hivyo kuchukuwa hatua kamili zitakazoboresha nchi na ulimwengu wetu.”

“Mazingira yetu yemedhalalishwa na mabwanyenye walio wachache wanaojihusisha katika ukataji mkubwa wa miti, uchimbaji madini na utumizi wa raslimali asili hivyo kutuwacha sisi walio hoi wengi kugharamia matendo haya kwa maisha yetu kutokeapo majanga,” Mauso alisema.

Hali kadhalika, wananchi wa kawaida wasikose kufanya chochote kile kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, haswa katika upanzi wa miti kwa vile hii ndio njia yenye gharama ya chini mno katika kupunguza adhari zake, kulingana na Mauso.

Mikakati ya kimazingira katika maeno enyeji

Mauso, aliyefanya kazi wakati mmoja na Wizara ya Fedha kama mwanauchumi mkuu, alisema kwamba anazitaka serikali zote duniani kukoma kuzungumzia swala la mabadiliko ya tabia nchi kijujuu tu, ila wayafanye kuwa rahisi kwa jamii enyeji kuelewa.

“Hapo awali, tulipokuwa mikutanoni na wanajamii, tungetumia majina kama vile mabadiliko ya tabia nchi na kupanda kwa halijoto duniani hivyo, wanavijiji wengi wangeondoka nje kwa dhana kwamba tunazungumzia maswala inayohusu watu wa tabaka la juu,” Mauso alisema. “Umakinifu wao tuliunasa punde tulipoweza kuijanibisha na kuwaeleza ya kwamba upanzi wa miti ni kwa manufaa yao wenyewe.”

“Kutokana na motisha iliyotokana na kikundi hiki, nafikiria kuanzisha sera itakayo saidia upanzi wa miti mingi nchini kote, lakini tunahitaji kuwa waangalifu ni miti anina gani; ni lazima iwe miti ya hali ya juu, kwa vile aina fulani ya miti haiwezi stahimili hali ngumu iliyoko maeneo ya milima,” alisema.

Iwapo hatua ya Nambeshe itazaa matunda, basi Uganda iko mbioni kujiunga na mataifa ya Rwanda na Kenya ambayo tayari yamepitisha sheria inayohitaji kila mwananchi anayemiliki nyumba kupanda angalau kiasi fulani cha miti.

Nambeshe, ambaye ni mbunge katika kamati ya mabadiliko ya tabia nchi bungeni, hata hivyo angependa kuona kuongezeka kwa nia kisiasa katika mapambano na mabadiliko haya, kutoka serikali ya Uganda.

Pia anatetea mikakati inayoendeshwa na jamii kama ile ya BECOMAP, kupokea usaidizi kutoka kwa serikali na washirika wa maendeleo ili kuwezesha ustawi endelevu.

Kulingana na Waziri wa Kitaifa katika Wizara ya Mazingira, Dkt. Mary Gorreti Kitutu, suluhu la kudumu dhidi ya maporomoko ya ardhi na majanga mengine huko Bugisu ni kuregesha mazingira yaliyodhalilishwa katika hali yao ya mbeleni.

“Janga la maporomoko ya ardhi itazidi kutendeka ikiwa wananchi watendelea kuzorotesha mazingira, huku wakiendeleza ukulima wa mbinu duni. Twahitajika kulinda vikingo vya mito,” alisema, akiongeza kusema kuwa vikundi vinavyojihusisha katika mapigano na mabadiliko ya tabia nchi kama vile BECOMAP lazima vihusishe wanawake na vijana katika juhudi hii.

Utafiti wa mwaka wa 2017 ulioendeshwa na taasisi ya Africa Natural Resources Institute, yadokeza kuwa uharibifu wa misitu umeongezeka kwa takriban hektari 200,000 kila mwaka nchini Uganda. Uharibifu huu unasababishwa kwa kiasi kikubwa na binadamu, huku kiasi kidogo tu kikitokana na sababu asilia, kulingana na ripoti.

Kwa upande mmoja, cha kulaumiwa ni ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini Uganda, ambayo inaongezeka kwa asilimia 3.6 kwa mwaka. Kufikia Agosti wa 2019, idadi ya watu nchini Uganda ilikuwa ni 45,883,274, kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa. Kiwango hiki kikidumishwa, basi kufikia mwaka wa 2025, Uganda itakuwa makaazi ya watu takriban milioni 63.

Sarah Netalisire, aliyekuwa muwakilishi wa kike bungeni eneo la Manafwa, ni mmojapo wa viongozi aliyeshauri waanzilishi wa BECOMAP. Anataka wazo la kikundi hiki kuigwa na jamii zingine nchini Uganda, zikiwemo zile ziko maeneo ya mijini.

Mwanasheria huyu wa zamani analitaka shirika la United Nations Intergovernmental Panel on Climate Change,  inayohusisha pia mabaraza nchini Uganda kama vile kamati ya bunge, mashirika ya kulinda mazingira yanayoongozwa na mamlaka ya National Environmental Mangagement Authority (NEMA) na kitengo cha kimazingira cha polisi, kuongeza juhudi zao.

“Wanastahili kuipa nguvu sera hii, ili kuwashurutisha watu kupanda miti katika mabustani yao, kando kando ya maboma yao, maeneo ya kazi na katika maeneo ya umma kama vile masoko na maeneo ya kuabudu,” Netalisire alisema.