Mabishano Ya Kinamasi Cha Yala: Ahadi  Zilizovunjika, Ardhi Imebakia Mahame

Ripoti hii imefanikishwa kwa ushirikiano wa InfoNile na Code for Africa na usaidizi kutoka kwa Pulitzer Center

Na Geoffrey Kamadi

Kisa kinachohusisha kinamasi cha Yala na kampuni ya Dominion Farms Limited huenda kikafananishwa na usimulizi mwingine wowote wa kusikitisha, ambao kwa kawaida uhusisha kitendo cha unyakuzi ardhi ambao umekwenda mrama. Mara nyingi, visa kama hivi uhusisha makampuni yenye uwezo mkubwa wa kifedha na jamii asili masikini.

Kuhusika kwa jamii katika mikataba aina hii kwa kawaida huwa ni mdogo. Majadiliano yeyote huwa inawahusisha wazee wawili au watatu wa kijiji walioteuliwa pamoja na wanasiasa.

Hivyo basi, haishangazi kuona kwamba utetezi wa matakwa ya wanajamii na viongozi hawa huwa hafifu, wa kimya, au wao (viongozi) huonekana kuegemea upande wa makampuni haya.

Hii hupelekea kutokea kwa nyufa kati na miongoni mwa jamii, kupotea kwa nafasi ya maendeleo, hasara chungu nzima ya uwekezaji na ahadi zilizovunjika.

Mwishowe jamii hujipata pale pale ilipokuwa kabla ya unyakuzi wa ardhi kufanyika, au hali yake huzorota zaidi kuliko ilivyokuwa mbeleni.

Kisa cha unyakuzi wa ardhi ya kinamasi cha Yala na Dominion Farms Limited sio tofauti na uelezaji huu. Matukio kama haya yaonekana kuchukua mkondo sawa katika kisa hiki. Mwanzo, kuhusishwa kwa jamii katika unyakuzi huu ulikuwa mdogo mno – chanzo muafaka wa uchochezi wa ugomvi.

“Njia zinazostahili hazikufuatwa,” asema Jacob Ouma, chifu wa kata ndogo ya eneo la Kadenge, Kaunti ya Siaya, ambayo imo ndani ya kinamasi hicho, mwendo wa masaa mawili kaskazini-magharibi wa Jiji la Kisumu. Anazungumuzia jinsi ambavyo kampuni ya Dominion Farms Limited ilibakia kumiliki ardhi ya kinamasi hicho.

Mwanzo, kabla ya kampuni hii ya uwekezaji ya Kimarekani kujitokeza, sehemu ya ardhi hii ilithibitiwa na mamlaka ya Lake Basin Development Authority (LBDA), ambayo husimamia maswala yote ndani ya Bonde la Ziwa Victoria.

Katika wakati huo, LBDA ilikalia upande wa kushoto wa ardhi hiyo, huku jamii ikiendeleza kilimo katika upande wa kulia.

Philip Oloo, mkurugenzi wa maswala ya kilimo na raslimali asili pale LBDA asema kwamba mamalaka haya hayakutekeleza majukumu yake kupitia umiliki kamilifu wa ardhi hii, kwa vile ardhi ilikuwa ya jamii. Ilishikiliwa tu kwa maumana na baraza la kaunti.

“Kinamasi hiki hakikutumika kikamilifu ipasavyo, hivyo basi kuhitajika kwa ushirikiano wa watu wengine ili kukiendeleza,” asema Oloo.

Basi hivyo ndivyo wazo la Dominion Farms Limited lilivyokuja. Muwekezaji alikodishwa ardhi ya kinamasi hiki kwa muda wa miaka 25 kwa uanzilishi wa miradi ya kilimo iliyohusisha ukuzaji mpunga, ndizi na muwa pamoja na uzalishaji pamba na samaki.

Serikali ya Kenya tayari ilikuwa kwishatoa tita la shilingi milioni 120 ($1.2 milioni) ambazo zilitumika kwa ujenzi wa lambo. Wakati huo huo, LBDA ililenga kukomboa hektari 12,000 kutoka kwa kinamasi ili kukiendeleza.

Mamlaka haya yalifanikiwa kukomboa hektari 2,000 katika awamu ya kwanza ya mpango huu. Katika awamu ya pili, mradi huu ulifaa kutekelezwa kwa ushirikiano na Dominion Farms Limited. Hata hivyo, haikutekelezwa kikamilifu, kwa vile zoezi hili lilihitaji ufadhili mkubwa wa kifedha.

Kutajika kwake kama mradi mkubwa zaidi wa uwekezaji wa aina yake katika eneo la Ziwa Victoria nchini Kenya, makusudio ya kilimo ya Dominion Farms yalionekana kama sisimko kubwa kwa uchumi wa Kaunti ya Siaya.

Kando na kubuni nafasi za kazi kwa wenyeji hapa, ilitarajiwa kuwa uwekezaji huu ungelisisimua uchumi mzima wa eneo la bonde la ziwa linalokumbwa na lindi la umasikini.

Hata hivyo, ili kukita kambi katika eneo hili la kinamasi cha Yala, lenye ukubwa wa kilomita mraba 200, ilibidi Dominion Farms Limited kukabiliana na changamoto ambazo kwa kawaida hukabili shughuli za upatikanaji ardhi. Ilibainika kwamba hili ni swala ambalo kampuni hii ilishindwa kulimudu, hivyo kupelekea kuzuka kwa migogoro kati ya wasimamizi wa kampuni na wenyeji.

Kutengwa kwa wenyeji ilidhihirika wazi kufuatia kusahihishwa kwa hati ya makubaliano kati ya kampuni hii na zilizokuwa mabaraza za kaunti za Bondo na Siaya. Mchango wa maoni ya jamii haikuzingatiwa, asema.

“Hii ilizua sintofahamu kubwa,” akumbuka, akiongezea kusema kwamba punde tu mradi huu ulivyoanza, faida yake ilikengeushwa. Mapato yake yalifaa kuregeshewa jamii.

Bwana Oloo ashiriki katika maoni haya.

“Mpangilio wa Dominion Farms kushirikisha jamii au LBDA, haukuwepo,” aelezea. Hivyo ni kusema ya kwamba muwekezaji huyu wa Kimarekani aliamua kumuweka kando mshiriki mkuu katika swala hili.

Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa Oloo, Dominion Farms haikuwatenga tu washika dau muhimu, ila kampuni hii iliamua kujishughulisha peke yake na kufanya kazi na mabaraza za kaunti za Bondo na Siaya.

Kutwaliwa kwa ardhi na kampuni hii, iliwaacha wenyeji bila ya maishilio. Hata hivyo, iliwalazimu kujipatia riziki kwa udi na uvumba. Hivyo basi, wenyeji waliingia katika kinamasi kwa lazima, huku wakikata mafunjo kutayarisha shamba kwa upanzi na uendelezaji wa ukulima mdogo.

Hata hivyo, waliondolewa punde baadaye. Hii ilisababisha takriban watu 6,000 walihamishwa, kulingana na Ouma.

Ingawaje ushinde huu wa unyakuzi ardhi uliwakasirisha wengi, kushutumu mradi huu wote kiujumla itakuwa unafiki, kwa upande mwingine. Ukweli wa mambo ni kuwa, baadhi ya miradi iliyotekelezwa na Dominion Farms, ilileta manufaa katika maisha ya wenyeji.

Kwa uhakika, baadhi ya shule zilinufaika kutokana na mipangilio ya kijamii iliyotekelezwa na kampuni hii. Miongoni ya shule hizi ni ile ya msingi ya Kanyaboli, Nyaluta na Obambo.

Kwa mfano, vilasi viwili vya shule ya msingi ya Gendro vilijengwa, pamoja na kurekebishwa kwa kiwanja cha michezo cha shule hiyo. Vigingi vya chuma viliwekwa katika kiwanja cha kabumbu badala ya vile vya mbao.

“Dominion Farms pia ilikusudia kujenga maabara ya kisasa katika zahanati ya Kadenge Ratuoro, ila kwa pingamizi kutoka kwa wenyeji,” asema Ouma.

Sababu ya shaka yao, aelezea Ouma, ilitokana na tetesi iliyotanda ikieneza dhana ya kwamba wazo la ujenzi wa maabara hayo ilikuwa tu njama ya Dominion Farms kuthibiti kikamilifu zahanati hiyo.

Veronica Ombwa, mtafiti wa kisayansi katika shirika la utafiti la Kenya Marine and Fisheries Research Institute (KMFRI) anasifu hicho ambacho kampuni hii ya Kimarekani ilikuwa inajaribu kufanya. Alijiujiunga na kampuni hii mnamo mwaka wa 2011kama mwanagenzi wakati alipokuwa akitafiti ukuzaji samaki wa kisasa.

“Ilifanya kazi ya kusifika katika ukuzaji tilapia na samaki aina ya kambare…ilikuwa na zaidi ya vidimbwi mia moja,“ aongeza kusema.

Anadokeza kusema kwamba, Dominion Farms ndilo shirika la kwanza kati ya mashirika mengine yote au mtu binafsi, lililotilia maanani utafiti wao. Hivi ndivyo ambavyo ukuzaji samaki kizimbani ulivyoanzishwa kikamilifu ndani ya Ziwa Victoria, mwaka wa 2005.

“Wenyeji walianza ukuzaji samaki kizimbani kwa vile tu kampuni hii tayari ilikuwa imeshaonyesha njia,” aeleza Ombwa ambaye ni mtaalam wa ukuzaji samaki kutumia mbinu za kisasa, akiwa na taaluma katika uchanganuzi wa elimu ya vijiumbe.

Kitu ambacho Ombwa hakukubaliana nacho ni kule kunyunyuzia dawa kutoka angani katika kinamasi hiki, ulioendelezwa na kampuni hii. Swali hili halikuwa mbali na fikra za watu wengi.

“Walilaumia kwa uchafuzi wa mazingira kwa kunyunyuzia madawa katika mashamba ya mpunga dhidi ya wadudu, magugu na ndege haribifu,” anakumbuka Ouma.

“Samaki walipatikana kama wameshakufa katika ile mifereji inayounganisha Mto Yala na Ziwa Kanyaboli, ambayo ni sehemu ya kinamasi hiki,” anasisitiza.

Umuhimu wa swala hili ilipelekea serikali ya mtaa, ikishirikiana na mamlaka ya Water Resources Management Authority (WRMA) pamoja na idara ya maswala ya samaki kuitisha utafiti ili kubaini ukweli wa madai haya katika mwaka wa 2010.

“Hata hivyo matokeo yake hatujayaona tangu wakati huo,” asema Ouma.

Umuhimu wa kinamasi hiki kimazingira hauwezi kusisitizwa kupita kifani, haswa ikizingatiwa jinsi ambavyo umewiana na usalama wa mazingira ya Ziwa Victoria kwa ujumla.

“Kinamasi hiki huwa ni kama kichungi kinachosafisha Mto Yala kabla ya kuyamwaga maji yake ndani ya Ziwa Victoria,” aeleza Dkt. Christopher Aura naibu mkurugenzi wa utafiti wa maswala ya mfumo wa maji safi katika taasisi ya KMFRI, kituo cha Kisumu.

Asema kwamba, kinamasi huondoa aina ya kemikali kama vile posferi, nitrati na kathalika, inapatikanayo katika madawa ya wadudu inayotumika katika mashamba iliyo karibu. Hutumika pia kama eneo la utegaji mayai na samaki aina ya kambare.

Ripoti ya KMFRI ya hivi karibuni ya kisayansi (itakayochapishwa hivi punde katika jarida la kisayansi ) inaonyesha kwamba mito miwili ipatikanayo kaskazini ya Ziwa Victoria ndiyo inayochangia pakubwa katika uchafuzi wa ziwa hili. Mito hii ni ile ya Nzoia na Mto Yala mtawalia.

Kiwanda cha kutengeneza karatasi kinapatikana kando ya Mto Nzoia na kampuni ya Dominion Farms inapatikana karibu na Mto Yala. Viwanda hivi huenda vinachangia katika uchafuzi, kwa mujibu wa Dkt. Aura.

Hata hivyo, uchafuzi unaochangiwa na Mto Sondu na Kuja, ipatikanayo kusini mwa ziwa, ni mdogo ukilinganishwa na uchafuzi utokanao na mito iliyoko eneo la kaskazini.

Matokeo ya utafiti huu yanalingana na utafiti mwingine uliochapishwa katika jarida la International Journal of Science and Research (IJSR) katika mwaka wa 2014.

“Utafiti unaonyesha kwamba, uharibifu wa raslimali ya kimazingira, kama vile utumiaji mbaya wa ardhi na mradi wa umwagiliaji maji wa Dominion, haiathiri tu kiasi cha huduma za kimazingira bali pia inaathiri ubora wa huduma hizi kando na kutoa changamoto kwa ukakamavu wa kinamasi kuhakikisha maendeleo endelevu ya watu wa Alego kusini ya kati.”

Mnamo mwaka wa 2018, Dominion Farms Limited iliondoka katika eneo hili, miaka 12 kabla ya muda wake wa ukodishaji ardhi kukamilika.

Hakuna shughuli zozote zinazoendelea kwa sasa. Kile unachokutana nacho hapa ni maghala marefu ya mpunga na kiwanda cha muwa ambazo zimekosa kazi. Hatua kwa hatua, majengo haya yanazorota.

Aidha, hakuna shughuli zozote zinazofanyika ndani ya karakana. Hata hivyo, uwanja huu umetapakaa na aina aina ya mashine nzito za kilimo, pamoja na matingatinga na majembe ya kulima.

Inastaajabisha jinsi vifaa hivi havitumiki, ikizingatiwa kwamba hali ya vifaa hivi bado ni nzuri na vinaonekana kuwa vipya.

Shughuli pekee inayofanyika hapa ni ile ya mifugo kula nyasi ama kutembea ovyo kati ya vifaa hivi. Kadhalika, kuna uwezekano mkubwa ya kuwaona akina mama wakiogesha wana wao huku ngozi zao nyeusi zikimeremeta, kando ya vijito vinavyojipindapinda hapa.

Hali inayanayojitokeza hapa inaonyesha mandhari ya kuvutia, ila tu kwa hali isiyo ya kawaida.

Oloo wa LBDA aeleza kwamba, mikataba ya ukodishaji ardhi hairuhusu utumiaji ardhi kwa shughuli zingine zozote kando na zile ambazo zilikusudiwa. Hii ni pamoja na kutoitumia ardhi kikamilifu.

Hii ni kusema kwamba, kutotumika kwa ardhi hii huenda ikasisimua hali ya kisheria, ambayo hatima yake itapelekea umiliki wa ardhi kuregeshewa wamiliki asili. Wakati ndio utakaoamua.


Mikataba ya unyakuzi ardhi nchini Kenya

Kama tu mataifa mengi barani Afrika, Kenya haijaepuka mshawasha wa kukodisha ardhi yake kwa makampuni ya kimataifa au serikali za kigeni. Wawekezaji hutumia ardhi hii kukuza chakula na/ au kwa uzalishaji wa mazao nishati kwa manufaa ya wananchi wao nyumbani au kwa faida ya kifedha.

Idadi ya mikataba ya ardhi iliyoidhinishwa na kukamilika nchini Kenya tangu mwaka wa 2000 ni 11. Hii ni kwa mujibu wa Land Matrix, ambao ni mpangilio huru wa kimataifa unaofuatilia mikataba ya ardhi ambao pia hudumisha uwazi na uwajibikaji katika maamuzi yanayohusu nyakuzi kubwa ya ardhi katika nchi zenye mapato ya chini nay a wastani ulimwenguni.

Mikataba miwili kati ya hii yote, ilitibuka baada ya kukamilishwa na kuidhinishwa. Mikataba ya ardhi yote miwili ya Dominion Group na Bedford Biofuels ilitupiliwa mbali.

Ikiwa na hektari 160 elfu zilizotengewa kwa mradi wake, Bedford Biofuels ndio unyakuzi mkubwa wa ardhi aina yake kufikia wakati huu, kulingana na kigezo cha Land Matrix, kinachofuatilia mikataba ya ardhi inayozidi hektari 200. Mradi huu ulikusudia kuwekeza katika ukuzaji wa mmea wa jatropha katika Delta ya Mto Tana.

Mkataba mdogo zaidi ulikuwa ule wa hektari 300 wa Asante Capital EPZ Moringa SCA SICAR. Uwekezaji wa kitita cha dola milioni 600 ulienda kwa ukuzaji wa mitishamba kama moringa na tangawizi pamoja na miti ya mkalitusi.

Hektari elfu sita zilizonyakuliwa na Dominion Group katika kinamasi cha Yala, ndani ya  Kaunti ya Siaya, zilinuiwa kwa miradi kadhaa ya ukulima. Miongoni mwao ikiwa ukuzaji mpunga, muwa na uzalishaji mseto wa kuku na samaki.

Kati ya mikataba ya unyakuzi ardhi, miwili tu kati ya hii yote ndio bado haijaidhinishwa. Hii ni pamoja na ile ya hektari 40,468 ya Arafco Agriculutural Integration Company Ltd inayomilikiwa na Prince Sultan Bin Nassir Bin Abdulaziz Al-Said wa Saudia.

Mradi huu ungeliwekeza dola milioni 216 katika ujenzi wa mradi wa muwa katika shamba la Galana lililoko jijini Malindi, pwani ya Kenya. Kubuniwa kwa mradi huu mwaka wa 2010, hatima yake haijulikani kufuatia migogoro miongoni mwa wawekezaji wake. Ni unyakuzi mkubwa wa pili zaidi kuidhinishwa nchini.

Halafu pia, kuna hektari 7,000 wa mradi wa Actis Capital LLP Craftskills Wind Energy International of Kenya. Likitarajiwa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 100, mradi huu uko mbioni kuwa wa pili mkubwa katika uzalishaji umeme utokanao na nguvu za upepo, nyuma ya ule wa megawati 310 wa Lake Turkana Wind Power.

Originally published in ScienceAfrica