Mushkeli katika sheria zachochea unyakuaji ardhi

Wawekezaji wa kigeni walipata hektari millioni 2.5 ya ardhi

Na Paul Jimbo

Makala haya yametayarishwa kwa hisani ya InfoNile na Code for Africa pamoja na usaidizi kutoka kwa Pulitzer Center

Sudan Kusini, nchi changa zaidi duniani, imekuwa ikigonga vichwa vya habaria ulimwenguni, sio kwa sababu nzuri, ila tu kwa sababu zinginezo zikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe, migogoro ya kikabila na unyakuaji ardhi.

Migogoro mingi ya kikabila hutokana na kupigania ardhi na raslimali za maji zinazopungua kila uchao, katika nchi ambayo umri wake ni chini mwongo mmoja.

Mahali palipo na ufukara wa juu na unyakuaji mkubwa wa ardhi ya jamii imewaacha wachungaji wengi kubakia na sehemu ndogo za malisho na kuathiri visima asilia. Uchungu wa unyakuaji holela wa ardhi haujasaza jamii enyeji, ambazo tegemo lao kubwa la maji ni Mto mkubwa wa Nile.

Ukataji wa miti uliosambaa kwa madhumuni ya kutoa nafasi kwa wawekezaji wa kibiashara imeathiri pakubwa ukingo wa Mto Nile uliosababishwa na kutumia maji yake kwa kilimo cha unyunyuziaji maji.

Kung’ang’ania  kwa ardhi kando kando ya Mto Nile ulioendeshwa na wawekezaji wa kigeni, kumepelekea ugawaji wa hektari nyingi za ardhi ya kijamii iliyo na rotba, bila ya kuhusisha jamii enyeji.

Hifadhidata Matriki ya Ardhi, ambayo hukusanya takwimu za unyakuaji ardhi kutoka kwa serikali, makampuni, mashirika yasiyo ya serikali, vyombo vya habari na mchango wa wananchi ulifuatilia takriban hektari milioni 2.5 ya eneo la ardhi lililonyakuliwa nchini Sudan Kusini, tangu mwaka wa 2006. Unyakuaji ardhi ni kule kujipatia ardhi bila ya kujali maslahi ya wanaomiliki haki ya ardhi hiyo.

Eneo kubwa la ardhi hii iligawiwa miradi 11 za kimataifa kutoka nchi za Falme za Kiarabu, Sudan, Norway, Uingereza, Saudia na Misri ambazo zilipata vipande vikubwa vya ardhi kwa ukuzaji mimea, uzalishaji mbao, unasaji kaboni pamoja na utalii.

Unyakuaji mwingi wa ardhi ulitendeka katika eneo la Equatoria na baadhi ya  maeneo ya Bah erGhazel. Unyakuaji mkubwa katika maeneo haya yalilenga uchimbaji wa raslimali, uchimbaji mafuta na kilimo, RT News iliripoti.

Katika mwaka wa 2008, kampuni ijulikanayo kama A1 Ain National Wildlife Company ya Falme za Kiarabu ilipatiwa kibali cha miaka 30 ya kujenga kambi za safari katika hektari milioni 1.7, pamoja na kujenga furushi la mandhari la wanyama pori ndani ya mbuga la wanyama la Boma National Park, ambayo ni mwenyeji ya mojawapo ya uhamaji mkubwa zaidi ya wanyama pori duniani.

Katika mwaka wa 2009, kampuni ya Misri ijulikanayo kama Qalaa Holdings, ilinyakua 105,000 ya ardhi iliyo bora kwa kilimo cha umwagiliaji maji ya Mto Nile kwa upanzi wa mimea inayosafirishwa hadi nchini humo, hii ikiwa mojawapo ya mikakati ya kutotegemea umwagiliaji maji katika bonde lenye rotba la Nile nchini Misri, kwa ukuzaji wa chakula chake chote.

Katika mwaka wa 2007, kampuni ya Norway ijulikanayo kama Green Resources ilinyakuwa hektari 180,000 katika jimbo la Central Equitoria kwa upanzi wa msitu ikitumia mti wa aina ya msaji, kwa kunasa kaboni.  Chini ya mpangilio wa kimataifa wa REDD wa kupunguza athari za tabia nchi, makampuni yanayo toa kaboni hewani, yanaweza nunua kaboni mkopo kutoka kwa yale ambayo hupanda miti kuondoa kaboni hewani.

Hata hivyo, upanzi wa aina moja wa mmea umeonyeshwa mara kwa mara kuwa na athari mbaya kwa mazingira na jamii asili. Ripoti ya taasisi ya Oakland Institute, iliyo na makao yake California, ilidhihirisha kuwa kampuni ya Green Resources ilifurusha jamii asilia, ikaizuia kupata maji na malisho huku ikitumia kemikali zinazoharibu mazingira asili.

Katika mipangilio mingine ya ardhi, mnamo mwaka wa 2010, mwana wa mfalme Prince Bandar bin Sultan Al Saud, aliyekuwa mjumbe maalum wa Abdullah, mfalme wa zamani na mkurugenzi mkuu wa shirika la kijasusi la Saudia, alinyakuwa takriban hektari 100,000 katika jimbo la Gwit ili kuendeleza kilimo.

Ardhi ya Nile yagawanywa

Ukisafiri kwa gari kwa takriban kilomita 10 kutoka Gumbo hadi barabara ya Rajaf, takriban kilomita 10 kusini mwa jiji la Juba, ilidhihirika kwamba vipande vingi vya ardhi kandokando wa Mto Nile imegawanywa kwa mashirika ya kigeni.

Katika maeneo mengine, vibao vilikuwa vimesimamishwa vikiwa na maandishi kama vile “mali ya” na “si ya kuuzwa” kuashiria umiliki wa kibinafsi. Vipande vingine vilivyotengwa kwa kutumia kuta za saruji, ingawa hapakuwa na ithibati ya shughuli za kilimo ndani vipande hivyo.

Vibao vingine viliandikwa kwa lugha ya Kichina, ikiashiria wazi jinsi ambavyo ardhi ya Mto Nile ilivyo ya kuvutia kwa wawekezaji kutoka mbali. Katika shamba moja la mboga, na eneo la biashara ya ujenzi maandishi yalisema, “Sheng DA, Mtaa wa Kichina, nambari 9, Gumbo, RajafPayam”.

Ndani ya boma hili, walikuwemo Wachina wa kiume na kike pamoja na majibwa weusi walioyokuwa na afya nzuri. Hawakuzungumza kiingereza, ila tu waliwashirikisha wafanya kazi wao kwa ishara za mikono. Walikuwa na mashine kubwa za kilimo, miongoni mwao, mashine kubwa za kuondoa vifusi ambazo zimeharibika, tingatinga za kulima na kuvuna: ambayo ni masalio ya vita vya 2016.

Kwa sasa, mashine hizi hutumika kwa ukulima mdogo mdogo wa mboga na kwa ujenzi wa matofali.

Vipande vya ardhi kama hivi vilipangika kwa foleni hadi kwenye ukingo wa Mto Nile.

Maboma ya mitaa mingine yalilindwa na walinda usalama waliojihami kikamilifu. Mitungi ya urefu wa hadi fiti 20 na fiti 40 yaliwekwa juu ya nyingine: vikiwa vifaa vya uhifadhi vinavyomilikiwa na makampuni ya kihamali.

Paulina Wani, mwenya umri wa miaka 48 na anayetoka kwa jamii ya Bari, alishutumu unyakuaji wa ardhi ya mababu zake.

Mama wa watoto saba, Wani alisema kuwa ardhi iliyoko Gumbo na Rajaf ni ya jamii ya Bari, hata hivyo, wamekuwa wakisukumwa kutoka kwenye ardhi hiyo tangu nyakati za vita vya miaka ya1980.

“Katika vita vya Anyanya 1 vya mwaka wa 1983, watu fulani walikuja hapa wakidai kwamba tuliwaficha waasi, kwa hivyo wakalivuruga kijiji. Baadhi yetu tulilazimika kuhama kutokana na mafuriko ya mto,” Paulina alikumbuka.

Ilikuwa wakati huu ambapo madalali walianza kulenga shamba lao lenye rotuba kandokando mwa Mto Nile.

Alisema kwamba, siku za hivi karibuni, baadhi ya wanasiasa na madalali waliidhinisha ukodishaji wa mashamba ya jamii yenye rotuba kwa mashirika ya kimataifa kuendeleza kilimo.

“Waweza amini kuwa hata wameshanyakuwa visiwa vidogo vilivyomo ndani ya mto? Visiwa vile vidogo vya futi 10 mraba unavyoona pale, vina wenyewe,” Paulina alisema akinyoosha kidole kuonyesha visiwa vidogo vya mawe-mawe.

Paulina, ambaye alisema kwamba babu yake alimiliki vipande vikubwa vya mashamba, sasa amebasalia na sehemu ndogo tu ya shamba ambamo yeye na jamaa yake wanaendeleza kilimo kidogo.

Baadhi ya wawekezaji wanaotengeneza sharubati na kukodisha mabohari wameshaingilia ukingo wa mto, kwa kusimamisha kuta za saruji hata kufikia maji ya mto.

Katika visa vingine, wawekezaji, pamoja na wale waliomo katika biashara ya hoteli wamejigawia ufuo ili kunufaika na biashara ya hoteli iliyo na faida kubwa huko Juba, ambalo ni jiji kuu la Sudan Kusini.

Kutokana na shindikizo kubwa la ardhi, Mto Nile imelazimika kubadilisha mkondo wake.

Kingo za Mto Nile zilizokwaruzika ni ithibati kuwa mto huu unajitahidi kupumua na kufurahia afya yake iliyokuwa nzuri zamani.

Mipango ya kupunguza ukosefu wa chakula kupitia kilimo biashara

Serikali inawahimiza wawekezaji wapya ikitarajia kwamba makampuni ya kigeni yatazalisha chakula hivyo kupunguza ukosefu mkubwa wa chakula, alisema Dk. Loro George Leju Lugor, mkurugenzi mkuu katika idara ya uzalishaji na huduma za kilimo yaani Agriculture Production and Extension Services.

Zaidi ya watu milioni 7.1 – ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya Sudan Kusini – wanahatarishwa na njaa, iliyosababishwa na hali mbaya ya kiuchumi, vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na ukame katika siku za hivi karibuni. 

Kwa mujibu wa Norwegian People’s Aid-South Sudan, muda hadi kufikia vita vya mwaka wa 2016, wawekesaji wa kigeni, miongoni mwao wale kutoka Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi za Uarabuni, walimiliki takriban asilimia 10 ya ardhi yote nchini kwa madhumuni ya kuchimba raslimali, mafuta na uzalishaji wa kilimo.

Hata hivyo, mnamo mwaka wa 2016 wakati vita vilizidi nchini Sudan Kusini, makampuni makubwa ya ukulima ya kigeni walihama nchi. Hivi sasa, nyingi ya mashamba hayo ni mahame.

“Tunavyoongea, robo tatu ya nchi itakumbwa na njaa kubwa kwa vile hatuna uzalishaji chakula wa kutosha. Hatuna mashamba yanayomwagiliwa maji kwa sasa, hakuna kilimo biashara, ambavyo tulikuwa navyo kabla ya vita vya mwaka wa 2016,” Leju alisema.

Hata hivyo, serikali imeweka mikakati maalum kuwashirikisha wawekezaji wakibiashara wakubwa kwa uzalishaji chakula kukidhi naskisi kubwa ya chakula. Mpango mkubwa wa ukame, mafuriko na kilimo yani 2014 Drought and Flood Vision Comprehensive Agriculture Master Plan, inatazamia uzalishaji wa kibiashara wa chakula kupitia wawekezaji nchini na wale wa kigeni, alisema Leju.

Hii itahusisha ukulima unaotegemea utafiti mwingi, ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula wa hali ya juu, alisema.

“Tumegawanya nchi katika sehemu sita za kiekolojia, kuhakikisha utosheleshaji wa chakula. Tuko na ukanda wa Nile, maeneo tambarare ya mashariki na magharibi, mabonde, milima, sehemu kame pamoja na maeneo ya kilimo na ekolojia,” alisema.

Leju asema kwamba serikali itaidhinisha kutumika kwa mashamba kwa shughuli za kilimo na malisho pamoja na kutengwa kwao kwa misitu hifadhi kitaifa, nchini kote Sudan Kusini.

Wizara pia inakarabati mashine za ukulima zilizoharibika, baadhi zao zikiwa za bei gali, alisema.

Anasema kwamba, jinsi ambavyo shamba linamilikiwa na jamii, huwa fursa ya jamii hii kuwa shabaha la walaghai wa mashamba nchini.

Kadri ambavyo serikali inapanga “kuwekeza pakubwa katika uzalishaji chakula kutumia wawekezaji,” “vile walivyojipatia ardhi sio jukumu letu kwa sababu kunao wanaoshughulikia maswala ya ardhi,” Leju alisema.

Ukosefu wa sheria kamili za mashamba

Migogoro ya mashamba inatokana na ukosefu wa sheria na taratibu kamili ya mashamba, baada ya Sudan Kusini kupata uhuru kutoka kwa Sudan kaskazini mwaka wa 2011, kwa mujibu wa Moses Maal, mkurugenzi mkuu mtendaji Wizara ya Ardhi, nchini Sudan Kusini.

Katika makubaliano mengi ya ardhi, manispaa ilikosa kulinda haki za wenyeji kwa kuwa watu hawa hawana stakabathi za umiliki ambazo zinatambulika na serikali kuu.

“Kwa mujibu wa katiba ya kabla ya uhuru ya Sudan Kusini, ardhi inamilikiwa na wenyeji – jamii. Hutumia ugawanyaji ardhi kuingia katika makubaliano,” Maal alisema.

Baada ya uhuru, sera za mashamba nchini Sudan Kusini ilirudishwa bungeni ili kuzungumuziwa, hata hivyo hakuna sheria mpya iliyopitishwa, Maal asema. Kwa sasa, nchi inategemea sheria ya kabla ya uhuru ya mwaka wa 2009 wakati kila jimbo lina sera, sheria na taratibu zake za ardhi.

Makundi haya matatu kwa kawaida ndiyo humiliki ardhi: jamii asili, serikali kuu na manispaa pamoja na wanaokodi mashamba wa kibinafsi.

Umiliki ardhi wa kijamii ndio mkuu zaidi, ambao unaruhusu jamii kutumia mashamba chini ya sheria asilia. Ardhi ya serikali kwa kawaida inaorodheshwa chini ya mbuga za kitaifa, hifadhi za wanyamapori na misitu.

Ingawa umiliki mashamba wa kibinafsi ama ukodeshaji mashamba wa kibinafsi unapatikana mijini mara nyingi, wawekezaji wa kigeni kama Green Horizon inayomilikiwa na Waisraeli, hivi karibuni wameonyesha dhamira kunyakuwa ardhi vijijini. Ardhi kama hii kwa kawaida hukodeshwa na jamii pamoja na taasisi za serikali.

Wawekezaji huchukuwa nafasi kujinufaisha kutokana na ukosefu wa sheria kamili za ardhi na kuingia katika makataa na watu na jamii  wasio makini, Maal asema.

Katibu mkuu wa kundi la South Sudan Land Alliance, Wodcan Saviour Lazarus alisema swala la ardhi lina mhemko mkubwa nchini Sudan Kusini, haswa baada ya vita vya miaka ya 2013 and 2016 ambavyo vilisababisha raia kukimbilia makazi salama kutoka makao ya mababu zao.

Mawakili huogopa kushughulikia kesi za mashamba na wao hukumbana na vitisho kwa vile migogoro ya mashamba kwa kawaida uhusisha “watu walio na ushawishi mkubwa” katika jamii, alisema.

Sheria ya mwaka wa 2009 inakumbana na ugumu wa utekelezaji kwa sababu raslimali watu na uwezo wa kifedha ni duni, alisema.

Miongoni mwa mashirika yaliopewa jukumu la kutekeleza Sheria ya Ardhi ni Payam Land Council, County Land Authority, State Land Commission na National Land Commission. Hata hivyo, Payam Land Council – mamlaka ya ardhi katika makaunti – haipo, na kama ipo huwa haina nguvu, Wodcan alisema.

“Sudan Kusini ilikuwa na majimbo 10 pekee kabla ya zogo la mwaka wa 2016, ambalo lilisababisha kubuniwa kwa majimbo 32 mapya. Hii ilileta mkanganyiko zaidi, kwa vile vikosi havina raslimali watu na nguvu za kifedha kutekeleza majukumu yao. Mtafaruku huu umepelekea baadhi ya majimbo, miongoni mwao koti za kiasili, kutekeleza sheria zao wenyewe,” Wodcan alisema.

Sheria ya 2009 inaruhusu makampuni kukodisha ardhi kwa muda usiozidi miaka 99. Hata hivyo, sheria ile ya Investment Promotion Act, ambayo pia ilipitishwa mwaka wa 2009, inaruhusu ukodishaji wa kati ya miaka 30 hadi 60.

Ili kuzuia mabishano zaidi, wizara inaweka mikakati ya sheria mpya nchini, Maal alisema.

Hata hivyo, harakati hii imekuwa ikiendelea: stakabathi za kusudio hili la kutengeneza sera ya ardhi nchini, ilikabithiwa Robert Lado, mwenyekiti wa South Sudan Land Commission mnamo mwaka wa 2014 na aliyekuwa naibu wa rais Riek Machar, katika mkutano wa baraza la mawaziri.

“Sera hii iliteua kanuni elekezi kadhaa, miongoni mwao ikiwa ile ya usalama wa haki za ardhi, usawa katika matumizi ya ardhi na kuwepo kwa usalama na aina tofauti ya muda za umiliki. Sera hii imegawanya ardhi katika makundi matatu: ardhi ya umma, kibinafsi na ile inayomilikiwa na jamii,” alisema maal.

Maal alisema kwamba serikali kuu inapaswa kuwajibika kwa maswala ya ardhi ya umma na kwamba taratibu ya kuwapa ardhi wawekezaji inapasa kuhusisha dhibitisho ya hiyo ardhi na serikal kupaswa kujulishwa kabla ya makubaliano kuafikiwa na mamlaka zinazohusika.

“Kwa wakati huu, wawekezaji unaowaona hapa, wanawadhulumu wenyeji kwa kurejelea makubaliano yaliyosahihiwa hata kabla ya sheria za ardhi kuwekwa,” alisema.

William Ebere Amosa, mtaalam wa maswala ya ardhi katika Wizara ya Ardhi za Kitaifa, alisema kuwa sera mpya sasa zinatambua umuhimu wa watu binafsi kumiliki mashamba na kuhakikisha usalama wa muda wa umiliki huo, jambo ambalo alisema ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Kwa miaka mitano sasa, stakabathi ya sera za ardhi imekaa tu katika bunge ikisuburi kuidhinishwa na bunge.

Hata hivyo, Musembe Glamourson, afisa wa programu katika shirika la South Sudan Land Alliance, alisema kuwa watu wengi hawajui kwamba miswada ya sera zipo, hivyo basi, ipo haja ya uhamasisho kamili punde mswada imepitishwa na kuratibiwa.

Kwa sasa, mswada uko katika usomaji wake wa tatu na huenda ukapitishwa mwaka huu, Glamourson alisema.

Katika mwaka wa 2013, baraza la mawaziri lilipitisha sera nyingine tofauti iliyosubiriwa kwa muda mrefu, ambayo ilikusudia kutatua maswala yanayohusu unyakuzi na udhibiti wa ardhi nchini.

Sera mpya ililenga kutatua migogoro ya baada ya vita inayosababishwa na haki za ardhi, vitongoji duni mijini, pamoja na migogoro itokanayo na upatikanaji wa mashamba iliyo na malisho na maji.

Inakusudiwa kuwa, unyakuzi wa ardhi na mitafaruku kuhusu mipaka kati ya makaunti na wilaya itatatuliwa na sera hii.

Upinzani mkali wa jamii, kwapelekea kubatilishwa kwa mkataba wa ardhi

Licha ya sheria zisizoeleweka, kuna visa vya wenyeji kufaulu dhidi ya dhidi ya unyakuzi wa ardhi nchini.

Mojawapo ya mikataba ya ardhi yenye utata mkubwa, na ambayo ilibatilishwa kufuatia upanzani ya wenyeji, ilisahihiwa mnamo mwaka wa 2008 kati ya kampuni iliyo na makao yake jijini Dallas, jimbo la Texas, kwa jina Nile Trading and Development na Mukaya Payam Cooperative.

Mkataba huu wa $25,000, uliyokodisha hektari 600,000 ya ardhi katikati mwa Sudan Kusini kwa kampuni hii ya Marekani kwa kipindi cha miaka 49, hivyo kukipa haki kamilifu zisizo na kifani za kuitumia ardhi kwa utafutaji wa mafuta, uzalishaji mbao na ukulima wa mashamba makubwa.

Baada ya ombi la kisheria la mwaka wa 2008, wenyeji wa Mukaya Payam walidai kuwa kampuni hii haikutafuta ushauri kutoka kwao na kwamba zaidi ya familia 600,000 zingefurushwa na mradi huo, hivyo ikapelekea kiongozi wa Sudan Kusini, Mtukufu Rais Salva Kiir kubatilisha mkataba huo.

Jemma Kiden mwenye umri wa miaka 30 alikuwa na miaka 20 wakati mkataba wa Mukaya Payam ulisahihiwa kijijini kwake. Anakumbuka vizuri jinsi ambavyo babu yake, pamoja na wazee wenzake walivyopinga unyakuzi wa ardhi.

“Kile tulichokiona ni magari ya kifahari na wageni wakizunguka katika mashamba yetu. Baadhi yao walikuw ni wazungu na wengineo raia wa Sudan Kusini, ambao hata hatukuwatambua,” alisema Kiden.

Kubatilishwa kwa mkataba ililenga kunufaisha wenyeji, alisema.

“Jinsi gani unaweza kugawa shamba la kijamii kwa malengo ya ubinafsi bila hata kutilia maanani maslahi ya wenyeji? Inanihuzunisha kuona jinsi ambavyo tama inavyotumiwa kufurusha watu,” Kiden alisema.

Charles Wani ni mkulima kutoka Lanya, mwendo mrefu magharibi wa jiji la Juba. Anasema alihamia kaunti ndogo ya Lanya, baada ya sehemu ya kipande chake cha shamba kilipogawiwa mkataba wa Mukaya Payam.

“Hatukuhusishwa kamwe. Hakuna aliyejishughulisha kutueleza kilichokuwa kinatendeka. Tulichokisikia ni kuwa, ardhi ya mababu zetu imepeanwa na kinachotia uchungu mwingi ni kwamba shamba hili liligawiwa wawekezaji wa kigeni kwa bei ya kutupa,” Wani alisema.

“Wajua vyema kwamba swala la ardhi zua hisia kali nchini Sudan Kusini. Ni vyema kwamba Rais aliingilia kati; mgogoro huu  ungebadilika kuwa zogo kubwa,” Wani alisema.

Ripoti ya ziada pamoja na uhariri umefanywa na Annika McGinnis